KWANINI SHERIA HAIWABANI WANAOKAA VITI VYA NYUMA KUFUNGA MKANDA?
Na Adrian mgaya
Shirika la afya duniani linataja viashiria vikuu vya ajali
za barabarani kuwa ni kutokuvaa kofia ngumu kwa waendesha pikipiki, mwendokasi
usiofaa, matumizi ya vilevi kwa madereva, kutotumia vizuizi vya watoto na
kutofunga mkanda wa usalama katika vyombo vya usafiri.
Pamoja na viashiria hivi kutajwa kuwa ni vyanzo vikuu vya
ajali na kuongezeka kwa madhara ya ajali za barabarani bado sheria mama ya
usalama barabarani nchini Tanzania, haijagusia kiundani mambo haya ili kuendana
na matakwa ya umoja wa mataifa kupitia shirika la afya duniani.
Ambapo wanapendekeza sheria madhubuti zitasaidia kupunguza
vifo na majeruhi wa ajali katika barabara zetu.
Edda sanga,
Mkurugenzi mtendaji wa TAMWA anasema "Umoja wa mataifa na shirika la afya
duniani wanakiri kwamba sheria madhubuti zinahitajika katika kupunguza
idadi ya watu wanaofariki katika barabara zetu. Tanzania lazima tuwe na sheria
kali za usalama barabarani kukomesha hali hii”
Sheria ya usalama barabarani ya mwaka 1973 ambayo ilifanyiwa
marekebisho mwaka 2002 nchini Tanzania, ina mapungufu ambayo kwa namna moja ama
nyingine hukwamisha mpango wa kutokomeza ajali za barabarani pamoja na madhara
yake.
Kwa mfano sheria ya usalama barabarani ya mwaka 1973 ambayo
ilifanyiwa marekebisho mwaka 2002 imewasahau kabisa abiria wanaokaa viti vya
nyuma, katika kifungu cha 39(11) kinatoa mwanya kwa abiria wa viti vya nyuma
kutofunga mkanda.
Kwa mujibu wa kifungu hiki dereva na abiria wa mbele ndio
wanaotakiwa kufunga mkanda huku wale waliokaa nyuma wakiachwa huru.
Ripoti ya mwaka 2015 ya shirika la afya duniani katika
masuala ya usalama barabarani inaeleza kuwa ufungaji sahihi wa mkanda
hupunguza madhara pindi ajali inapotokea zaidi ya ASILIMIA 50% kwa dereva
na abiria wa viti vya mbele na zaidi ya 75% kwa abiria wa viti vya nyuma.
Mary Kessi, mratibu wa mradi maalumu wa usalama barabarani
nchini Tanzania kutoka shirika la afya duniani, ofisi za Dar es salaam, ambapo
kwa sasa wanashughulika na mabadiliko ya sheria za usalama barabarani,
anasema...
"Unapokuwa umefunga mkanda unakuwa salama zaidi pindi
ajali itakapotokea tofauti na usipofunga”…
Anaendelea kueleza kuwa "tumeshirikiana na wadau
mbalimbali tumeweza kufanya utafiti na kubaini kuna mapungufu katika sheria
zetu, hivyo tunaishauri serikali kufanya marekebisho katika sheria ili kuondoa
baadhi ya mapungufu", anasema.
Utafiti huu unaungwa mkono na takwimu za ajali za barabarani
zinazotolewa na jeshi la polisi kikosi cha usalama barabarani.
Ambapo mwanasheria wa jeshi la polisi kikosi cha usalama
barabarani ASP Deus Sokoni anaweka wazi
kuwa madhara huwa ni makubwa zaidi pindi ajali zinapotokea wale wasiofunga
mkanda hupata madhara makubwa ukilinganisha na wale waliofunga mkanda.
Tarehe 28 ya mwezi Mei 2017 ni siku ambayo imeacha historia
kwa Jasmin Mdoe shabiki wa timu ya Simba ambaye alikuwa katika gari ndogo
binafsi lililopata ajali maeneo ya Dumila, Morogoro wakitokea Dodoma.
Jasmine anaeleza kuwa wakiwa wanatoka kuangalia mchezo wa
soka kati ya Simba na Mbao wakiwa na furaha tele baada ya timu yao (Simba)
kuibuka na ushindi katika mchezo huo uliochezwa mjini Dodoma, furaha yao
iligeuka majonzi ghafla.
Gari walilopanda lilipasuka gurudumu la mbele na kupinduka.
Jasmine anaeleza kuwa ajali ile ilikatisha Maisha ya rafiki yake aliyejulikana
kwa jina la Shose Fidelis, na rafiki zake wengine wakiachwa na majeruha.
“Shose, alikaa kiti cha nyuma kabisa na hakufunga mkanda.
Sisi wengine tulifunga mikanda, licha ya gari kupinduka mara tatu ila tulibaki
katika viti vyetu,” anasimulia Jasmine Mdoe.
Licha ya hatari inayoweza kutokea, baadhi ya abiria
wanaotumia magari binafsi hawafungi mikanda ya usalama hasa wanaokaa katika
viti vya nyuma kutokana na sababu mbalimbali,
Lakini huenda sheria ingekuwa na sehemu inayolazimisha
kufunga mkanda kwa abiria wote jambo hili jambo hili lisingekuwepo.
Ras Lumelezi mkazi wa Bagamoyo anasema“mimi naona kuna
umuhimu wa kufunga mkanda kwa sababu huwezi kujua dereva anaeendesha hilo gari
amelewa, au hilo gari linaweza kuwa na hitilafu ya kiufundi”
Vilevile anaeleza “ajali inaweza ikatokea muda wowote,
lakini kuna vitu ambavyo tunaweza kuchukua kama tahadhari ikiwemo kufunga
mikanda, hata kama ajali itatokea basi madhara yasiwe makubwa…”
Kwa upande wake Musa Jumanne mwanafunzi wa darasa la tano
katika shule ya msingi Assumption mkoani Arusha anasema kuwa kila siku asubuhi
anatumia usafiri wa daladala kwenda shule lakini siku zote huwa anapata
kigugumizi “Dereva na abiria wa mbele wanafunga mkanda nashangaa kwanini
wasiweke mikanda na viti vya nyuma?” anauliza Musa Jumanne.
Kwa mujibu wa ripoti ya usalama barabarani yam waka 2015
iliyotolewa na umoja wa mataifa kupitia shirika la afya duniani Tanzania ni
miongoni mwa nchi za ukanda wa afrika mashariki zilizo na sheria ambayo haigusi
abiria wote katika suala la ufungaji mkanda wa usalama.
Nchi za Kenya na Uganda zinatajwa kuwa na sheria
madhubuti inayowataka abiria wote wawe wamefunga mkanda ambayo huenda inabana
watumiaji wa magari kutofunga mikanda ya usalama. Swali ni lililo vichwani mwa
wengi ni lini Tanzania itakuwa na sheria imara katika ufungaji wa mikanda.
Mwanahabari mkongwe ambaye kwa sasa anafanya kazi
Televisheni ya Taifa TBC 1, Tuma Provian Dandi yeye ni muathirika wa ajali za
barabarani, anasema “pamoja na kuwa kuna sheria za usalama barabarani, lakini
nina imani zingine zimechakaa” …
Anaendelea kusema… “mathalani sheria ya kufunga mkanda
inamuamuru dereva na abiria wa mbele wawe wamefunga mkanda, nadhani imefika
wakati sasa hii sheria ifanyiwe marekebisho yaani iwe kosa kwa abiria yoyote
kukaa kupanda gari bila kufunga mkanda”
Ukimya sheria ya usalama barabarani juu ya umuhimu na
ulazima wa kufunga mkanda wa usalama kwa abiria wa viti vya nyuma si tu
unawanyima abiria haki ya kujilinda bali unaongeza idadi ya utegemezi kwa
waathirika wa ajali za barabarani,
Na ndio maana asasi mbalimbali za kiraia kama vile TAMWA,
TAWLA, SHIVYAWATA, Road safety ambassadors(RSA), AMEND na Tanzania Lawyers
Society (TLS) zimekuwa zikipigia kelele mabadiliko ya sheria.
Mabhezyo Rehani mwanasheria kutoka Tanzania Lawyers Society(TLS)
anaeleza kwamba “Sheria yetu ipo kimya juu ya ufungaji mkanda kwa abiria wa
nyuma,”
“na unaweza ukaona sheria mama inakinzana na sheria nyingine
ambazo zimeshakuja mbele ya sheria mama ambazo zinagusia abiria wote wale wa
mbele na wa nyuma, kwa hiyo ni vizuri pia sheria mama ikaaweka ulazima wa
abiria wote kufunga mkanda”.
Kauli hii inaungwa mkono na mwenyekiti wa mabalozi wa
usalama barabarani nchini John Seka ambaye anaona mabadiliko ya sheria, yanaweza
kupunguza madhara yanayotokana na ajali za barabarani kutokana na kutofunga
mkanda.
Mchakato wa mabadiliko ya sheria ya usalama barabarani
haukwepeki, mwenyekiti wa kamati maalumu ya kurekebisha sheria ya usalama
barabarani, ambaye pia ni wakili na mwanasheria wa jeshi la polisi ASP Deus
Sokoni, anaeleza kuwa hatua zote katika mchakato wa kubadilisha sheria za
usalama barabarani zikikamilika zitapelekwa bungeni Bungeni ili kuridhia
iwe sheria.
Hata hivyo mbali na sheria ya usalama barabarani kuwa na mapungufu
bado watumiaji wanatakiwa kuangalia zaidi usalama wao kwa kuzingatia kufunga
mkanda, kwani wahenga walisema kinga ni bora kuliko tiba
Makala hii imeandikwa na Adrian Mgaya mhitimu wa chou kikuu
cha Dar es salaam, katika shahada ya uandishi wa habari (B.A in Journalism)
ambaye ni mnufaika wa mafunzo ya uandishi wa habari za usalama barabarani
katika mradi wa WHO bloomberg initiative for global road safety,yanayoendeshwa
na Tanzania Media Foundation (TMF) anapatikana kwa 0656110670 au mgayaadrian@gmail.com
Comments
Post a Comment